HISTORIA YA SAYYID HUSSEIN BADAWY

HISTORIA YA SAYYID HUSSEIN BADAWY Al-habib Al-Alim Al-Fannan Sayyid: Hussein bin Ahmad Al-Badawy Swaleh bin Alwy bin Abdallah bin Hassan Al-Qaadhy bin Ahmad bin Abdallah [Swahib Tuyyur] bin Ahmad bin Harun bin Abdul-Rahman bin Ahmad bin Abdallah bin Shaykh Muhammad Jamali layl bin Hassan Al-Mua’llim bin Muhammad Asadullah Bin Hassan Al-Turaaby bin Ali bin [Faqiihul-Muqaddam] Muhammad bin Ali Ba’alawy bin Muhammad [Swahibul-Mirbat] bin Ali [Khali-Qassam] bin Alwy bin Muhammad [Swahib-Sawma’ah] bin Alwy bin Ubeidillah bin [Al-Imam Al-Muhajir Ila-llahi] Ahmad bin Issa An-Naqib bin Muhammad Jamaludiin bin Ali Al-Ureidhy bin Ja’afar Al-Swadiq bin Muhammad Al-Baqir bin Ali [Zain Al-Abidin] bin Hussein Al-Sibtwy bin Ali bin Abi Twalib,vile vile Hussein Al-Sibtwy bin Fatma Al-Zahra bint Rasuuli llah [S.A.W].( Abu Abdillah) Babake ni: Sayyid Al-Imam Ahmad Al-Badawy bin Al-Habib Swaleh bin Alwy Jamali Layl (Mwenye Badawy) Mamake ni: Bi Qamar bint Muhammad Al-Amoudy Sayyid Hussein alikuwa akijulikana kama “Abu Abdillah” na sababu ya kuitwa hivyo ni kuwa: safari moja Sayyid Hussein alikuwa yuwatembea na babake Mwenye Badawy hapo yeye ni mdogo kama miaka sita hivi na ndie alikuwa mtoto wa kutembea na babake saa zote,siku hiyo Sayyid Hussein akamwambia babake “baba we umenipa jina la Hussein na Husseini wote wamekonda ,Hussein Muhdhar amekonda,Hussein Mwiwa amekonda sasa mimi silitaki tena hili jina nibadilishie” basi Sayyid Ahmad Badawy akacheka sana na akawa huwatolea watu kiswa hicho kila mara.kisha sayyid Ahmad Badawy akamwambia mwanawe Sayyid Hussein basi kuanzia leo wewe ni “Abu Abdillahi” ambayo ni kun’ya ya Al-Imam Hussein As-Sibtwy (AS) Shariff Said bin Abdallah Al-beidh aliposikia jina hili la “Abu Abdillahi” basi maishani mwake hakujaaliwa kumuita Sayyid Hussein jina lingine,alikimuita “ Abu Abdillahi” kwa hadithi hiyo mpaka kufa kwake. Sayyid Hussein alipata bahati kubwa sana ya kupendwa na watu wakubwa na kupewa majina mengi ya lakabu,mfano Al-habib Ahmad Mash’hur bin Twaha Al-Hadad (Shariff Hadad) alikimuita “Al-muwafaq” kwa tabiya yake ya kuwafikiwa katika kila jambo analolikusudia kufanya,naye Sayyid Umar bin Abdallah (Mwenye Baraka) alikimuita “Naashiru Twariqati – Alawiyah” (yaani mwenye kueneza Twariqa ya Alawiyah) kwa Qaswida zake za mabwana watukufu na tabia zake njema. Sayyid Hussein alizaliwa tarehe 25 mwezi wa sita (June) mwaka wa 1933 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) na alizawa katika mtaa wa Riyadha kisiwani Amu (Lamu),na akapata malezi mema kutoka kwa wazazi wake wawili Sayyid Ahmad Badawy na bi Qamar, malezi mema na yaliyo sheheni ucha Mungu na elimu japo kuwa hakupata kumjua babake kwa uzuri sana kwani babake aliaga dunia Sayyid Hussein akiwa na umri mdogo sana miaka sita kwa hakika. Sayyid Hussein akaendelea kupata malezi kutoka kwa mamake na ndugu zake wakubwa haswa Sayyid Abdul-Rahman Khitamy (Shariff Khitamy) akimpenda sana bali alimchukua na kumueka nyumbani kwake na kumpa malezi mema pamoja na kumsomesha,Sayyid Hussein alikuwa na ndugu wengi sana kwa jumla wote walikuwa 21 lakini kwa upande wa mamake walikuwa watano yeye Sayyid Hussein,Sayyid Alwy (Mzee Mwenye),Sayyidah Maimunah,Sayyidah Zainab na moja alikufa udogoni. Sayyid Hussein Alisoma Quran kwa Sayyid Umar Al-Aidid na Shaykh Ali Swabu- ambae alikuwa ni mwanafunzi wa babake Sayyid Ahmad Badawy,kisha akasoma Tajweed kwa Shaykh Abdul-Rahman Bwana Ami – ambae nae alisoma kwa Sayyid Alwy bin Abubakar Al-Shatiry (Mwenye wa Makkah) huyu Mwenye wa Makkah ndiye aliyechukua Tajweed kutoka Makkah kwa Ijaaza na kutuletea huku kwetu. Shaykh Abdul-Rahman Bwana Ami ndiye aliyempa Sayyid Hussein ufaswaha wa Qurani na mengine mengi maanake Tajweed ina mambo makubwa sana baada ya kujua Tajweed kuna na kusomeshwa mapokezi tangu kwa Mtume (saw) na haya yote Sayyid Hussein aliyasoma na kumaliza kwa mwezi moja tu na hapo alikuwa akishirikiana na mwanafunzi mwenzake ambae alikuwa mzuri kwa upande kwa Tajweed akiitwa Shaykh Muhammad Twalib na walikuwa wakimaliza kusoma kwa Shaykh wao wanaenda katika msikiti wa Liwali Seif na huko wakisomeshana na kutwalii kwa pamoja. Sayyid Hussein alipoanza kusoma kwa Shaykh Abdul-Rahman Ami alikuwa kwanza hamtoi makosa kabisa mpaka pale Sayyid Hussein alipomuita kando na kumuuliza “mbona mimi hunitolei makosa kama wanafunzi wengine?,” Shaykh Abdul-rahman akamwambia “ nitakutoleaje kosa na babako ni Shekhe langu?”, Sayyid Hussein akamuuliza “basi huku ndiko kumlipa,kutonitolea kosa?” ,basi Sayyid Hussein asema nilipoanza kutolewa makosa nilihisi nikama sijui Qurani,lakini akaninyosha ulimi wangu na kunichonga kisawasawa kwa muda wa mwezi moja akanipa ufaswaha wote aliyopokea kutoka kwa Shekhe wake na alipomaliza kunisomesha, shahada kubwa aliyonipa ni kuniambia “sasa kasome popote ulimwenguni hauta tolewa kosa”. Na kweli neno hili lilithibiti pale alipokuja ziyara nchini Kenya bingwa wa ulimwengu katika usomaji wa Qurani kwa Tajweed “Shaykhul-Quraai” Mahmud Khalil Al-Hussary wa kutoka Misry alipokuja Malindi na kabla ya yeye kusoma akawataka wasomaji wa Kenya wasome kwanza,basi kila aliyesoma Shaykh hakukubali Qiraa chake mpaka aliposoma Sayyid Hussein Qiraa cha mwalimu wake Abdul-Rahman Ami lakini kwa sauti ya mwenyewe Hussary alipomaliza kusoma,Shaykh Hussary alikuwa amekaa na Al-imam Ar-Rahil Sayyid Muhammad Al-beidh akamuuliza “huyu amesoma wapi?”, Sayyid Muhammad akamwambia “Lamu”,Shaykh Hussary akamuuliza “Lamu ni wapi,huyu hajasafiri kwenda Misry?”, Sayyid Muhammad akamwambia “haja safiri kuenda Misry”,Shaykh Hussary akasema “lau kana fii Misry la-yundwar’{yaani huyu lau angelikuwa Misry angeangaliwa vizuri kwa maana angelipwa vizuri} kisha Shaykh Hussary akamuuliza Sayyid Muhammad “huyu huku kwenu ulipwa pesa ngapi kwa mwezi kwa usomaji wake?”, Sayyid Muhammad akamwambia “husoma bure” Shaykh Hussary akasema “basi huyu yuko katika zama za maswahaba”,kisha akampa Sayyid Hussein kishale chake kama ishara ya kukubaliwa kisomo chake na kuwa pia ni Ijaaza kabisa. Walipokutana tena Unguja (Zanzibar) Sayyid Hussein akasoma tena na hapo Shaykh Hussary amemsahau,alipomaliza kusoma Shaykh Hussary alimpa Sayyid Hussein barua ya masomo ya bure (Scholarship) ya kuenda Misry kuongeza maarifa yake katika elimu ya Qiraa na Tajweed lakini kwa bahati mbaya yalipotokea mapinduzi ya Zanzibar mnamo mwaka wa 1964 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) mambo yote yakaharibika. Sayyid Hussein baada ya kupata mafunzo mema ya Qurani na Tajweed aliingia katika nyanja ya kutafuta elimu ya dini na alipo palenga kwa ajili ya elimu ni Madrasa-tu-Najaah chuo kilichokuwa kimeasisiwa na babake Sayyid Ahmad Badawy na Shaykh Mahmud Fadhil mwaka wa 1934 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) na akasoma kwanza kwa ndugu zake wakubwa wake na waliokuwa wametalii vyema elimu hiyo nao ni pamoja na: - Al-Allamah Sayyid Ali Badawy - Al-Allamah Sayyid Muhammad Diin (Shariff Diin) - Al-Allamah Sayyid Abdul-Rahman Khitamy (Shariff Khitamy) - Al-Allamah Sayyid Hassan Badawy (Al-Muthaqqaf) - Al-Allamah Sayyid Alwy (Mzee Mwenye) Na pia akasoma kwa Mpwa wake (Nephew) Al-Allamah Sayyid Muhammah Bahassan mtoto wa ndugu yake mkubwa Sayyid Ali Badawy,na japo kuwa alikuwa ni mpwa wake lakini alikuwa ni mkubwa wake kiumri kwa takriban miaka minane na alimsomesha somo la Faraidh na Fiqhi. Sayyid Hussein pia akapata fursa ya kuendeleza masomo yake kwa wanazuoni wengine tajika waliokuwepo kisiwani Amu (Lamu) na nchi jirani ya Tanzania nao ni kama: - Al-Allamah Shaykh Muhammad bin Ali Al-Maawy - Al-Allamah Sayyid Muhammad Adnan Al-Ahdal - Al-Allamah Sheikh Muhammad Sheikh - Al-Allamah Shaykh Hassan bin Amiir Al-Shiraazy (akiwa Dar-es-salaam) -Al-Allamah Shaykh Ramadhan Abbas (akiwa Dar-es-salaam) huyu ndiye muasisi wa Madarasatul-Abassiyah Dar-es-salaam na pia akapata tarbiya,irshaad na muongozo wa kiroho kutoka kwa wacha-Mungu waliokubalika kama vile: - Al-Arif bi-llahi Al-Allamah Al-Habib Umar bin Sumeit - Al-Arif bi-llahi Al-Allamah Al-Habib Ahmad Mash’hur bin Twaha Al-Hadad (Shariff Hadad) - Al-Arif bi-llahi Al-Allamah Al-Habib Said bin Abdallah Al-Beidh (Shariff Saidi) -Al-Arif bi-llahi Al-Allamah Al-Habib Umar bin Abdallah Aalu-Sheikh (Mwenye Baraka) na wengineo. Sayyid Hussein alipokuwa bado yuwasoma Madrasatu Najaah alikuwa pia amepatiwa jukumu la kusomesha yaani mwalimu msaidizi na aliendelea na kazi hiyo mpaka mnamo mwaka wa 1950 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) alipoowa hapo akiwa na miaka kumi na saba na alimuowa binti wa ki-sharifu akiitwa Sayyidah Mwana-Fatma ambae alikuwa ni kutokana na ukoo wa Al-ahdal kwa upande wa baba na kwa upande wa mama binti huyo alikuwa ni kutokana na ukoo wa An-Nadhiiry na harusi hiyo ilifanyika kisiwani Rasini. Sayyid Hussein baada ya kuowa na kwa ugumu wa maisha kisiwani lamu,na ikieleweka kuwa Madrasati Najaah ilikuwa hakuna malipo kabisa,Sayyid Hussein kwa ajili ya kutafuta maisha ilibidi aondoke kisiwani Amu mnamo mwaka wa 1951 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) na kuhamia nchi jirani ya Tanzania katika mji wa Dar-es-salaam na alipofika huko akapokelewa vizuri na Shaykh Hassan bin Amiir Al-Shiraazy ambae kwa wakati huo alikuwa Dar-es-salaam kwa da’awah lakini ni mwenye asili ya Unguja (Zanzibar) na pia akapokelewa na Maalim Ramadhan Abbas ambae ni mwanafuzi wa Shaykh Hassan Al-Shiraazy na ndiye mwanzilishi na muasisi wa Madrasatu-Abbasiyah ilioko mjini Dar-es-salaam. Sayyid Hussein baada ya kufika Dar-es-salaam alipelekwa sehemu inayoitwa Kissiju Rufiji kwa ajili ya da’awah na huko akakaa kwa muda wa miezi sita huku akisomesha,kisha akarudi zake Dar-es-salaam na kupewa kazi ya kufundisha shule ya Jumuiyah katika barabara ambayo hapo mwanzo ilikuwa ikiitwa “New Street”, na baada ya muda mfupi Shaykh Liwali Ahmad Swalehe akampa Msikiti ambao ulikuwa hauswaliki kwa hali yake mbaya na Sayyid Hussein akaanza kuujenga na ukaimarika na akauita Masjid Badawy na akafungua Madrasa na kuiita Madrasa-tul- Badawy Mkunguni Dar-es-salaam na akawa hapo ndipo anaposomesha. Mnamo mwaka wa 1963 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) Sayyid Hussein alilazimika kuondoka Dar-es-salaam baada ya Serikali kumuamuru afanye hivyo na hii ni kwa sababu Madrasa yake “Madrasa-tul-Badawy” ilipoanza kufana na kuvuma ikawapelekea wakristo waliokuwa mtaa huo kuona kuwa Uislamu umeanza kushamiri na kupata nguvu na ushirikiano umeanza kuwa mzuri baina ya waislamu wa Dar-es-salaam,Zanzibar na Kenya ikizingatiwa Mombasa na Lamu,basi hapo kukapangwa njama ya kuondolewa Sayyid Hussein na waliopanga ni wakristo wakishirikiana na baadhi ya waislamu ambao walikuwa wanaona Sayyid Hussein ni tishio kwa malengo yao ya kibinafsi,wakafanya mkutano na kuamua kuwa huyu mtu “yaani Sayyid Hussein” hatumtaki hapa ndipo akatolewa. Sayyid Hussein kabla ya kuondoka Dar-es-salaam watu wanaompenda yaani wapenzi wake walikuja kumtaka ushauri kuwa “Shariffu tupe rukhsa tuipendue Serikali?”, maanake kando na wale watu kumtaka Sayyid Hussein aondoke Dar-es-salaam yeye pia alikuwa akipinga namna ya uongozi wa aliyekuwa Rais wa Tanzania kwa wakati huo Mwalimu Julius Nyerere na sio yeye pekee bali pia wanazuoni wengine walikuwa wakilipinga hilo kama vile: Shaykh Hassan bin Amiir Al-Shiirazy,Shaykh Nurdiin bin Hussein Al-ghassany Ash-shadhily na wengineo,na hawa wote pia walitolewa, Shaykh Hassan akarudishwa kwao Unguja (Zanzibar) na Shaykh Nurdiin kwa kuwa alikuwa ni Mtanzania asili alihamishwa Dar-es-salaam na kupelekwa Mgombezi Korogo. Wale wapenzi wa Sayyid Hussein walipokuja na kumuuliza kuwa “Shariffu tupe rukhsa tuipendue Serikali?”,hapo gari za vita vimeanza kuzunguka pale na ving’ora vina lia kila sehemu ikawa mapinduzi imekaribia,Sayyid Hussein akawambia “mi sikuja kuipendua serikali nimekuja kwa Usilamu,ikiwa nyinyi mwataka kuniombea ni baki niombeeni kiislamu sio kivita,kwanza mimi sijui vita,sijui mambo ya kupendua serikali wala sina daraja ya waziri wala cheo chochote kila,mimi ni muislamu”. Kisha Sayyid Hussein akarudi zake kwao Amu (Lamu) na mnamo wa 1963 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) Sayyid Hussein akaondoka Lamu na kuelekea Unguja (Zanzibar) na huko akapokewa vizuri sana na Al-Habib Umar bin Sumeit pamoja na ndugu yake mkubwa Sayyid Ali Badawy ambae kwa wakati huo alikuwa ni mwalimu wa chuo cha Ma’ahad Islamiyah Zanzibar “The Muslim Academy of Zanzibar”,na alipofika Sayyid Hussein akafunguliwa chuo katika Msikiti wa Majamvi Mkwajuni na akawa yuwasomesha hapo mpaka yalipopatikana mapinduzi ya Zanzibar mnamo mwaka wa 1964 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) na katika kipindi hicho Sayyid Hussein alipata taabu sana mpaka kutiwa gerezani kwa muda kwa kiswa kirefu ambapo hapa sio mahali pake. Sayyid Hussein alipowachiliwa na hali ikatulia kidogo Zanzibar,alimuendea Al-Habib Umar bin Sumeit kumtaka ushauri ya kuhamia nchi jirani ya Uganda kwa ajili ya da’awah maanake ilikuwa imekuja ombi kutoka kwa watu wa Uganda na hapo ni baada ya kufariki Shariff Saidi ambae ndiye aliyekuwa ameishika Uganda,Al-Habib Umar akampa rukhsa ya kuenda Uganda japo kuwa watu wa Unguja bado walikuwa wanamtaka.Sayyid Hussein alikuwa na uhusiano mzuri sana na Al-Habib Umar bin Sumeit na alikuwa kila jumamosi akienda nyumbani kwake kumuimbia Samai na Al-Habib akifurahiya sana. Sayyid Hussein mnamo mwaka wa 1964 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) kwa amri na ishara ya Al-Habib Umar bin Sumeit akaenda Uganda sehemu za Arua mpakani mwa Sudan na Zaire na akawa ni badali ya Shariff Said bin Abdallah Al-beidh,na kwa amri ya Al-Habib Umar bin Sumeit alipofika huko akajenga Masjidul-Hudaa na Madrasatul-fauzi wa Salaam na akaweka Taasisi (Institution) ya Jumuiyah Fauz wa Salaam ambayo ilikuwa imejumuisha Msikiti na Madrasa na akafanya kazi kubwa sana na akaishi huko kwa takriban miaka 17. Sayyid Hussein kisha mnamo mwaka wa 1981 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) akatoka Uganda na kuingia Sudan na sababu ya kutoka Uganda ni kwa kuwa ilikuwa kuna vita baina ya ma-rais wawili,Rais Iddi Amiin wa Uganda na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania ndipo akatorokea Sudan na kushukia katika kambi ya wakimbizi sehemu iitwayo Rijaaf na hapo akaanza kusomesha wale wakimbizi waliokuwepo katika kambi hizo na hii ni kwa kutotaka kukaa bure. Kisha mnamo mwaka wa 1982 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) Sayyid Hussein akatoka Sudan na kuelekea Zaire sehemu za Bunya na huko akajenga Msikiti na Madrasa na kuziita Masjiid Twaiba na Madrasatu-Twaiba vilevile akajenga na nyumba za waalimu na akafanya kazi kubwa sana huko,pia akafungua hoteli na akaiita “Zahir Hotel” kwa kufananisha na jina la Zaire na akanunua mashamba za kulima ili zote hizi zipate kusaidia Msikiti,Madrasa,wanafunzi na Waalimu sio kwa lengo la kupata pato la kidunia. Kisha Mwaka wa 1985 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) Sayyid Hussein akatoka Bunya yeye na rafiki yake akiitwa Shaykh Jambek na wakaenda sehemu iitwayo Goma karibu na mpaka wa Burundi hukohuko Zaire na huko wakajenga Msikiti uitwao Masjid Abraar maanake huo mtaa alioshukia ulikuwa ukiitwa Berere akafanya kama tash’bihi (Abraar na Berere) na akaishi huko kwa takriban miaka miwili na kwa muda huo wote akawa anasimamia Madrasa na Misikiti ya Bunya na Goma huko Zaire mpaka mwaka wa 1990 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) ambapo alirudi kwao Lamu. Sayyid Hussein aliporudi kwao Lamu kwa wazee wake alikuwa amerudi kwa niyyah ya kustaafu sasa ataka apumzike na kungalia maisha yake na hapo ndipo wakaja watu wa Lushoto Tanzania wakamuomba aje asimamie Madrasa ya Lushoto na akapewa Ardhi yenye heka 9 na nusu,Ardhi ambayo ilikuwa haina offer lakini Sayyid Hussein akaiendea mbio ikapata offer na akatia vigingi kwa gharama zake mwenyewe,maanake kiwanja hicho kilikuwa chataka kuchukuliwa na Serikali. Sayyid Hussein hapo alipofika Lushoto nchini Tanzania mwaka wa 1990 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) palikuwa ni msitu na kulikuwa kuna kijumba kidogo ndio akaifanya ni Madrasa hapo,kisha akajenga Madrasa na Workshop na nyumba ya waalimu na bweni la kulala watoto na hapo ndipo ilipotoka Madrasatul-Irshaad na akajenga Msikiti na kuuita Masjid Badawy na lengo la kujenga workshop ni kuwa baada ya mtoto kupata elimu nyingi ya dini pia apate kujua kazi za mkono iliapate kijikimu kimaisha.Sayyid Hussein pia akajenga Nursery ya kuwasomesha watoto Skuli ili watu wapate kujua na kutalii vyema elimu zote mbili ya dini na dunia,na bado ana niyyah ya kujenga Zahanati,Hospitali na Madrasa ya wanawake. Chuo hicho cha Lushoto kina wanafunzi wa kulala zaidi ya 100 kwa sasa na wakuenda zaidi ya 100 pia na wote wanasona bure bila malipo ya aina yoyote na yote hii ni bidii na mbio anazozienda Sayyid Hussein,vilevile chuo hicho kinatoa kila mwaka wanafunzi ambao wamemaliza masomo katika fani mbali mbali kama vile: udereva,useremala,ujenzi,ufundi wa umeme,elimu ya dini na vilevile kupeleka wanafunzi nchi za Arabuni kwa ajili ya kuzidisha masomo yao kama vile Hadhramut nchini Yemen na wakwanza walioenda na wakamaliza masomo huko ni kama Al-ustadh Abdallah Daud na Al-ustadh Ma’amun. Sayyid Hussein kwa kule kuhama hama kwake sehemu tofauti kwa ajili ya da’awah amewafundisha wanafunzi wengi sana wasiokuwa na idadi lakini tutajaribu kuwa taja japo kwa mukhtasari,itakumbukwa alipokuwa akifundisha Madrasatu Najaah Lamu ndiye aliyekuwa mwalimu wa Al-Imam Sayyid Muhammad bin Shariff Said Al-beidh na alimsomesha Qurani mpaka akahitimu na alipohitimu Shariff Said alimtunukia Sayyid Hussein Shillingi elfu 40 na akamwambia “hii ni ijara yako yaani malipo yako kwa kunisomeshea mwanangu” na alipokea pesa hizo kwa Shangazi mtoto na siku hizo ukipewa elfu 40 ni pesa nyingi sana waeza fungua duka nazo ama ukafanya mambo mengi sana nazo. Vilevile Sayyid Hussein ndiye aliyemfundisha Sayyid Muhammad Al-beidh khat na mabaadi’I zote (yaani maanzilishi ya masomo) pamoja na Sayyid Ahmad bin Ahmad Badawy (Mwenye Baba) ambae ni ndugu yake mdogo kwa baba,na watoto wake pia. Sayyid Hussein alipokuwa sehemu za Kisiji Rufiji aliinua sana usomaji wa Qurani huko na dalili ya natija hiyo utaiona kupitia wanafunzi wake kama vile: - Al-ustadh Adam - Al-ustadh Al-hady - Al-ustadh Abdul-khaliq ambae yuko Abu Dhabi - Al-ustadh Ismail Muhammad- muanzilishi wa Firqatu- Salaam (Dar-es-salaam) - Al-ustadh Abdallah Dawud ambae yuko London, na kwa kupitia hawa na mfano wao Dar-es-salaam iling’ara kwa ujuzi wa kuweza kusoma Qiraa’a mbalimbali kwa sauti tofauti tofauti kwa kupitia kazi,ujuzi na harakati za Sayyid Hussein. Katika maajabu ya Sayyid Hussein nikuwa aweza anza kufundisha mwanafunzi tangu “Alif” yaani Qaaidah mpaka akawa Qaari mkubwa sana. Sayyid Hussein ni Mshairi wa ajabu sana na ametunga mashairi mengi sana kwa lugha ya kiarabu na Kiswahili pia na katika uhodari wake Sayyid Hussein awaze fasiri mashairi ya Kiarabu kwa lugha ya Kiswahili tena kimashairi kwa namna ileile na bahari ileile na kwa sauti ileile.Sayyid pia alitunga baadhi ya vitabu kama vile: - kitabu cha Nahwu- ambacho ni sherehe ya Ajrumiyah - kitabu cha Fiqhi – ambacho amechambua na kufafanua zaidi - kitabu cha Mabaadi’i - kitabu cha Adhkar - kitabu cha Mashairi yake ya Kiswahili na kiarabu lakini zote hizi hazikupata bahati ya kuchapishwa. Sayyid Hussein ndiye Swahibul-Maqam wa Riyadha Lamu na aliwachiwa nafasi hii na ndugu yake mkubwa mlezi wake Sayyid Abdul-rahman Khitamy (Shariff Khitamy) na pia akausia kuwa akifa Sayyid Hussein ndiye amswaliye na pia Sayyid Muhammad bin Shariff Said Al-beidh aliusia hivyo hivyo kuwa aswaliwe na Sayyid Hussein na ndiye aliyewaswaliya wote kwa kutekeleza wasia wao. Sayyid Hussein badawy pia aliasisi madrasa na msikiti sehemu inayoitwa Yombo Dar-es-salaam na ndio taasisi yake ya mwisho na bado zaendelea na akaiita (yambu'ul-badawy) kwa kupigia Fali jina la yombo.na mwenye Hussein Badawy alikuwa akisema kuwa akipata afya atafanya kazi zaidi ya Dini kuliko alivyofanya katika ujana wake. Sayyid Hussein sehemu zote hizo alizotembea alikuwa akifundisha bure kutoka jadi,na hadi hii wa leo hana mshahara wowote ila nikutarajia ridhwaa ya Mola wake (swt) lakini Mwenyezi Mungu alimlipa malipo ya juu zaidi chochote akitakacho hupata bila hata kuitisha nikupe mfano amehijji hijja zaidi ya 30 na anasema hakuna aliyolipa na pesa zake mwenyewe,yeye ustukia tu ashafanyiwa kila kitu yeye ni kusafiri tu,Sayyid Hussein katika kuzunguka kwake kwa ajili ya da’awah ameishi sehemu tofauti kwa miaka tofauti mfano: - Aliishi Dar-es-Salaam kabla ya kufukuzwa miaka 12 - Aliishi Unguja (Zanzibar) mwaka moja - Aliishi Uganda miaka 17 - Aliishi Zaire miaka 15 - Na sasa ameishi lushoto miaka 30 Pamoja na miaka yote hiyo Sayyid Hussein na utu-uzima wake bado anayo ndoto na niyyah ya kufungua chuo cha kuwafundisha waalimu namna ya kufunza,maanake asema “watu wengi ni wasomi lakini hawajui namna ya kufunza na kuwaelewa watoto”, na yeye Sayyid alikuwa akisema kuwa “watoto wanatafautiana kuna mtoto ukimpeleka kusoma hafahamu hata akisomeshwa,na kuna wengine ufahamu maramoja akifundishwa,sasa haya ni mambo waalimu watakikana wayajue utawasomesha vipi?”, kisha akisema “kuna njia za kuwasomesha wote hao sio kupigana na kutukanana,we fuata ile tabiya ya mtoto na masomo yake mpe kadri ya uwezo wake,na utaona kila mwaka atazidi kupanda kielimu na atakapo zidi huwa na fahamu nzuri zaidi kushinda wale wengine”, alikuwa akisema kuwa “haya nikatika mambo waalimu hawayajui na yatakikaniwa wayajue sio vita tu kila saa”, na ndio akawa na niyyah ya kutaka kufungua chuo ama kutunga kitabu cha kumuelekeza mwalimu kufahamu usulubu huo.na pia alikuwa na ndoto ya kufungua chuo chenye kufundisha masomo za pande zote mbili dini na dunia kwa lugha ya kisasa (intergrated) ili mtu akipata shahada iwe ni shahada yenye kutambulika serikalini na hata katika mashirika yasiyokuwa yaki serikali. Sayyid Hussein katika maisha yake alipokuwa amechoka na mambo ya hapa na pale alitaka kuhamia Madina kwa Mtume [saw] na akawashauri Al-habib Umar bin Sumeit,Al-Habib Ahmad Mash’hur bin Twaha Al-Hadad (Shariff Hadad) na Shariff Karama aliyezikwa Nairobi sio Yule wa Mombasa,na wote hawa hawakumjibu ila Al-Habib Umar bin Sumeit alimwambia kuwa Madina inayo mwenyewe nenda ukamuombe yeye akikusudia Mtume (saw). Sayyid Hussein akatengeza makaratasi ya Hijra yaani kuhama kwa rafiki yake na wakaenda Makkah,walipofika huko makaratasi yake yakashikwa na bwana mmoja kisha wao wakamuambia Yule bwana kuwa huyu yaani Sayyid Hussein ataka kuhamia Madina,Yule bwana akawaambia kuwa jana mimi nilimuona Mtume usingizini akaniambia “huna ruhusa ya kuhamia huku kwa kuwa kule kwenu watu bado wananufaika na wewe,lakini ukihamia huku utanufaika wewe pekee bora ni lipi? Na huyu “yaani Sayyid Hussein” bado kazi yake haijaisha”. Nani kweli kauli ya Mtume (saw),maanake tangu Sayyid Hussein kuregea huku amejenga Misikiti mingi sana na pia ameasisi Madaaris nyingi sana. Sayyid Hussein Badawy aligonjeka kwa muda na alikuwa akiugua maradhi ya Sukari (Diabetes) ambayo mara kwa mara ilikuwa ikimkatiza safari zake na kwanza akakatwa kidole cha mguu kisha baada ya muda akakatwa mguu na pole pole akaendelea kudhohofika ki-afya akawa hawezi safari za mbali kisha akawa hata kutoka nje hawezi akawa sasa yeye ni mtu wa kitandani tu na mwishowe akapatwa na maradhi ya Baridi kuu upande wa kulia (paralysed) mpaka Mola alipomukhitari asubuhi ya siku ya Jumatano tarehe 27 mwezi wa mfungo tisa (Jumadal-Akhira) mwaka wa 1442 kulingana na kalenda ya kiislamu (Hijriyah) sawa na tarehe 10 mwezi wa pili (February) mwaka wa 2021 kulingana na kalenda ya kizungu (Miladiyah) na hatimaye kulazwa katika malazi yake ya milele walikolazwa wazee wake kwao kisiwani Amu (Lamu). Sayyid Hussein alikuwa akiwapenda watu wema sana na akiitakidi nyendo zao na malipo aliyopata ni ya kumtosha kwa kushikana na kusuhubiana nao,vilevile alishakana na nyendo za wazee wake na salaf wake mpaka utu-uzimani mwake,alikuwa mwenye tabia nzuri mcheshi kwa wote, hakudharau uwe mkubwa ama mdogo atakupa maskizi unayotaka na atakujibu kwa jawabu utakayo ridhika nayo na hivi ndivyo alivyoishi maisha yake yote, mpole asiyependa utata wala ugomvi na aliyependa kuunganisha sio kutatanisha,mwenye subira ya hali ya juu sana na imani kamilifu na Mola wake(swt) pamoja na mahaba na mapenzi ya dhati kwa Mtume,maswahaba,waumini na ndugu zake wote kwa jumla. In Shaa Allah kwa haya machache Mwenyezi Mungu amrehemu na amjaalie pepo ya Firdausi kuwa ndio makazi yake pamoja na wema waliotangulia,na atupe nasi Baraka zao na siri walizokuwa nazo mabwana wakubwa hawa ili nasi tuweze kufuata nyayo zao na kuiga mifano yao. Imeandikwa na kutayarishwa na ndugu yenu #Hussein Al-Moddy.

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA YA MAREHEM SHEKH MUHAMMAD MUSSA MZIMBIRI (1959 - 2020)

WANAUME WENGI WAKIJA KUFANIKIWA HUBADILIKA NA KUNYANYASA WAKE ZAO